in

AMKA MAMA: SIMULIZI YA KUSISIMUA NA KUHUZUNISHA

Amka Mama ni Simulizi Ambayo ina Sisimua na Pia Inafundisha. Moja kati ya Simulizi zitakazo Kuacha na Funzo Kubwa Katika Maisha. Soma Mpaka Mwisho Utafahamu Sababu ya Binti Huyu Kumuamsha Mama yake. Je, Alikufa, au Amelala Muda Mrefu. Ungana Nami Mwandishi wako @aisha-mapepe Kufahamu.

Amka Mama

SIMULIZI ZA MAISHA: AMKA MAMA.

“Kwako mama.”Sauti ya kike ilianza kwa kutoa salamu”.

Sauti yako bado imetawala kichwa changu licha ya kutoisikia kwa muda mrefu. Nakumbuka mengi uliyoniambia kuhusu maisha haya.

Maisha yaliyojaa Chuki, Manyanyaso, Wivu usio na kifani pamoja na dharau hata kwa wale ambao umewazidi. Kwa sababu wanacho,wanaona huwezi kuwaambia chochote. Nayakumbuka mengi sana mama yangu. Sauti chovu na ya kukata tamaa ikichanganyika na simanzi iliendelea kujieleza mbele ya mwili ambao iliamini kuwa unasikia akisemacho. Aliendelea

*********

Sidhani kama wajua ni kiasi gani nateseka kwa sasa, ila nafahamu wewe ndio mwenye kujua uchungu wa mwana na Unaumia sana kwa jinsi mimi niumiavyo. Japo hunioni ila naamini wanisikia, na ninajua unaufahamu wa kuyatambua haya maumivu yanayonikabiri kwa sababu yako.

Nayatoa haya kinywani mwangu huku nikikukumbusha yale uliyowahi kuniambia siku nyingi za nyuma wakati nipo karibu nawe, na wakati ulikuwa unaongea. Ulisema haya huku akianza kwa kuniita mwanangu na mkono wako wa kuume ukikipapasa kichwa changu, Mwanadada yule alianza kurudia maneno ya mama yake aliyoambiwa kipindi cha nyuma.

Bado hujayajua maisha yanaenda vipi japo wajua haya tunayoishi ndiyo maisha. Maumivu niyapatayo kwa ajili yako, kamwe huwezi kuyajua hadi wewe utakapopata mtoto wako.
Wewe ni sehemu ya tumbo langu, kaa ukitambua hilo. Kitovu chako, ni utumbo wangu. Nilichokula mimi na wewe ulikila kwa kupitia utumbo wangu.

Uliyasema haya mama na hukuishia hapa tu! Uliendelea.

“Wakati nimekubeba tumboni, kama mimi niliumwa, basi nilihofia sana kuhusu wewe kuliko kuumwa kwangu. Niliyajua maumivu unayoyapata ni zaidi ya mara zote ya ninayoyapata mimi. Nilijitahidi kujihudumia ili nikutoe katika maumivu niliyokubebesha, mwanangu. Kijana yule wa kike alimaliza kunukuu maneno ya mama yake kipenzi, kisha akaendelea.

Sikujua uliyasema haya kwa nini mama, lakini najua uliyasema katika kufikisha hisia zako kwangu, hisia ambazo kila mzazi wa kike anapaswa kuwa nazo kwa mwanaye.

*********

Sasa nimekuwa mkubwa wa kuyachanganua mambo ambayo ulikuwa ukiniambia. Lakini licha ya ukubwa nilionao, najua bado nikiumia hapa nilipo na niendako, wewe unaumia zaidi yangu. Wewe ni zaidi ya kila kitu katika maisha yangu. Naomba utambue hili.

Sitaki kujiuliza ni mara ngapi umepigana kwa ajili yangu kwani hata nikijua, siwezi kulipa wala kugusa pale ulipopita wewe. Ni kazi kubwa umeifanya mama yangu, na hii ni kwako mama. Inuka na futa chozi langu kama ulivyolifuta kipindi kile nilipokuwa nalitoa kwa sababu ya maumivu.

Hekima na busara zako ndizo zilizojaza ujasiri moyoni mwangu hata kwa yule ambaye niliwahi kusema sitamsamehe katika maisha yangu. Nataka kukwambia kuwa, nimemsamehe baba na huko alipo, MUNGU amlaze mahala pema peponi.

Japo najua alikuwa akikutenda sana,lakini ulisimamia kidete haki zako. Hata pale alipokupiga usiku wa manane na kukutaka uondoke nyumbani kwake, bado ulinikumbuka na kunikumbatia ili uondoke nami. Naikumbuka sana ile siku. Nilikuwa nina miaka sita. Ni zamani sana, kwani leo ninamiaka 28. miaka 22 imepita tangu tukio lile litukie.

Siku ile ilikuwa ni Jumapili kwa kuwa tulienda kanisani mimi na wewe. Sikumbuki ilikuwa ni tarehe ngapi, lakini ilikuwa ni mwezi wa kumi na mbili.
Tulipotoka kanisani na kurudi nyumbani,hatukumkuta baba. Naikumbuka ile siku,nakwambia tena hilo. Binti aliendelea kukumbusha anayokumbuka.

*********

Baba alirudi sijui saa ngapi, ila kilichonishtua usiku ule ni kusikia sauti yako ikilia huku mwili wako ukitoa sauti kama ya mtu anayekung’uta vumbi nguo zake.

Nilishuka kitandani ili nije kuona ni nini kinachoendelea usiku ule wa saa tisa na dakika kadhaa. Wakati huo hali ya hewa nje ilishabadilika sana. Wingu jeusi lilitanda, na manyunyu ya mvua taratibu yalianza kusikika kwenye paa la nyumba yetu.

Baada ya kutoka chumbani mlipokuwa mnanilaza, nilikuja hadi pale sebuleni na nilishuhudia kwa macho yangu baba akikuburuta sakafuni huku akikushindilia mateke katika mwili wako kana kwamba anamfanyia hivyo mnyama,au kitu chochote ambacho hakina uhai.

Hakika mama ile picha haijafutika katika kichwa changu. Yale mateke na ngumi alizokuwa anazishusha katika mwili wako,hadi sasa hivi picha ile inatawala ubongo wangu.
Hakika mama nakwambia, sijasahau hata chembe japo hukuwahi kuliongelea suala hili. Dada yule mrembo aliongea haya na safari hii machozi yalianza kutiririka toka machoni mwake lakini hakuacha kuongea japo sauti iliambatana na hali ya kilio.

Mama, nashindwa kufahamu nimeumbwaje,ila namshukuru MUNGU kaniumba jasiri kama wewe.
Nilipokiona kitendo kile, nilichomoka kwa kasi na kwenda kushikilia miguu ya baba aache kufanya alichokuwa anakifanya. Lakini kwa akili ambayo alikuwa nayo usiku ule, baba alinisukuma kama mpira wa miguu na mimi nilidondokea pembeni huku nikimuacha akiendelea kukuburuta pale sakafuni.

*********

Sikutaka kukubali kuendelea kukuona unazidi kufanyiwa matendo yale ya kikatiri na mtu ambaye ulimthamini hadi ukamkabidhi maisha yako ayaendeshe.

Nilisimama tena na kwenda kumkamata miguu baba na safari hii niliongezea kumng’ata ili aache kukufanyie yale.
Maumivu yaliyotokana na meno yangu kuingia katika ngozi yake, baba alijikuta akinipiga teke la nguvu tumboni na kunifanya nitoe mlio wa uchungu. Uchungu ambao hakuna ambaye angeuhisi zaidi yako wewe mama.

Na uchungu wangu huo ndio ulikupa ujasiri wa kuinuka pale chini na kumkunja baba kama mtoto mdogo. Baba alipojaribu kujitutumua ulizidi kumfundisha heshima iliyomtoka baada ya kubwia pombe zake. Heshima ambayo kama angekuwa nayo, asingethubutu kunipiga teke lile wala kukuthurubu wewe.

Hakika nakwambia mama. Wewe ni zaidi ya Komando,wewe ni zaidi ya wale wanaoweza kupindua nchi. Wewe ni zaidi ya kila kitu katika hii dunia. Naomba upokee hizi thamani nazozitoa mdomoni kwangu.

Amka mama, pigana hadi mwisho.Pigania pumzi yako.Nakuhitaji mama, nakuomba amka. Amka na kuniangalia mwanao, niangalie navyotaabika bila ushauri wako. Niangalie tena,amka mama, tafadhali. Binti yule aliongea hayo kwa uchungu huku akimtikisa mama yake aliyekuwa kalala kitandani katika wodi ya wagonjwa mahutihuti.

Bonyeza iyo Button Hapo Chini Iliyo andikwa Next Kutaza Sehemu inayo Fuata ya Simulizi Hii Amka Mama.

Written by Aisha Mapepe

Aisha Mapepe ni Mwandishi wa Simulizi Mbalimbali za Mapenzi, Maisha na za Kuelimisha. Lengo ni Kuburudisha Jamii na Kuondoa Stress za Maisha zinazo tukabili Baadhi Yetu.

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Akufukuzaye Akwambii Toka

AKUFUKUZAYE AKWAMBII TOKA: ASHURA NA BATULI

Sarafina Simulizi

SARAFINA: MOJA KATI YA SIMULUIZI PENDWA MNO