in

AMKA MAMA: SIMULIZI YA KUSISIMUA NA KUHUZUNISHA

*********

Mipira ilikupita puani na mdomoni huku akiwa hajielewi hata kidogo. Alikuwa ni wa kulishwa na mipira, kupumua kwa mipira na wa kujisaidia hapohapo.

Sasa mtoto wake anajaribu kuongea maneno makali ili kama mama yake yule kipenzi anasikia, aweze kuamka. Lakini kitendo kile cha kumtikisa mama yake kwa nguvu huku akifoka na kulia, kilipelekea wauguzi waje kumnyanyua pale alipokuwa kapiga magoti na kuanza kumtoa nje.

Niacheni niongee na mama yangu.Nasema niacheni mimi,niacheni. Binti yule alizidi kung’aka wakati anatolewa chumba kile na wauguzi waliokuwepo zamu.

Kuna nini jamani? Mbona kelele hivi. Kama sio hospitali bwana. Aliongea mzee mmoja wa makamo ambaye alikuwa amevalia mavazi nadhifu ya kiuguzi.
Ni huyu binti anampigia kelele mgonjwa,daktari. Alijibu muuguzi mmoja aliyekuwa anasaidiana na muuguzi mwingine kumtoa binti yule mule ndani.

Simpigii mgonjwa kelele, ninaongea na mama yangu. Niacheni tafadhali, niacheni nikaongee na mama yangu. Nawaombeni. Binti yule aliweka uso wa huruma mbele ya wale wauguzi watatu ambaye mmoja alikuwa ndiye Mganga mkuu (Daktari mkuu).

“Kama ni mama yake,muacheni akaseme naye kwa njia yoyote. Si mwajua ni mwezi wa tano sasa huyu mama hajielewi hapo kitandani.

Saa nyingine tutumie njia za kiimani kumponya mgonjwa hasa utabibu wetu unapokuwa unagonga mwamba. Mimi naamini kama mwanaye ataongea, basi mama huyu atasikia hasa mwanaye akiongea kwa upendo.

Muacheni akaongee naye,lakini binti usipige kelele, hapa ni sehemu ya wagonjwa, sawa mama? Muuguzi mkuu alitoa ruhusa na mara moja binti yule aliachiwa huku akimshukuru kwa kumpigia magoti kwa kumfanya arudi tena na kuongea na mama yake.

*********

Samahani mama kama nimekukosea. Nisamehe kwa lililotokea. Binti yule aliomba msamaha huku akifuta machozi na kamasi chache alizokuwa amezitoa wakati anaongea na mama yake pamoja na pale wauguzi walipokuwa wanamtoa nje ya chumba kile.

Nakumbuka ulinifundisha kuomba msamaha pale ulipohisi nimekosa. Siwezi kuacha hii tabia ya kuomba msamaha kwani ndiyo imetukuza mimi na wewe pale baba alipotufukuza kwa ukali katika nyumba uliyodumu nayo kwa miaka kumi na sita kama mke wake. Kwa sababu hiyo, siwezi kusema alikufukuza kwake bali alitufukuza nyumbani kwetu.

Lakini sababu gani baba alitufukuza nyumbani kwetu? Ni swali ambalo sikulipatia jibu hadi pale niliposikia ameondoka duniani.

Siku ile kama unaikumbuka vizuri, ulizipata taarifa za kifo cha baba asubuhi na mapema. Wewe kama mkewe uliyefunga naye ndoa halali kanisani,ulijifunga kipande cha kitenge kikuu kuu lakini kwako kilikuwa ndicho kina afadhari. Ulinikamata mkono wangu wa kulia, na moja kwa moja safari ya kwenda nyumbani ikashika hatamu baada ya miezi nane tangu tufukuzwe na baba.

Ulipofika pale wengi walikunyooshea vidole vya mashaka pamoja na visununu ambavyo vilionekana wazi vikitawala katika nyuso zinazoelezea nyoyo zao.
Hukuwajali bali ulijali kuwa unaenda pale msibani kama mke halali wa marehemu, mke mwenye uchungu na mume aliyeishi naye kwa miaka kumi na sita.

Uliniacha pale nje na wewe uliingia ndani ambapo ndipo baba alikuwa amehifadhiwa. Sijui kilichotokea ndani,ila baada ya dakika kadhaa,ulitolewa kwa nguvu na wanandugu wa upande wa baba yangu, Mzee Ched Tambo.

*********

Namkumbuka baba yangu, na nimeshamsamehe. MUNGU akurehemu. Binti yule iliinama kwa muda kama mwenye kusali kabla hajaamka na kuendelea kuongea na mama yake.

Sijui wale ndugu wa baba walikuwa na akili gani hadi wakafikia kusema wewe ndiye umeroga baba. Hivi ni kweli kabisa wewe ndiye ulimroga au yule mwanamke wake mpya ndiye alimpa sumu? Hilo swali sijawahi kukuuliza kama unalijua au hulijui, ila nafahamu unajua nini kiliendelea sema ulifunika kombe ili mwanaharamu apite.

Mama mbona mimi sijawahi kukuona ukijishughulisha na mambo ya kishirikina? Mbona katika makuzi yangu,sijawahi kukuona ukishika tunguri au hata kuvaa kishirikina ni kwa nini wale wakina shangazi na baba zangu walikutuhumu kwa hilo? Au walijua kuwa wewe ndiye utakuwa mrithi wa mali zile na ndio maana walikuchafua? Kwa nini walifanya vile?

Ni maswali ambayo huwezi kunijibu hata kama ungekuwa waweza kuongea. Lakini mimi ninamajibu yote. Najua wao ndio walipanga kifo cha baba yangu wakishirikiana na yule mwanamke mpya ambaye ndiye aliyemchanganya baba hadi usiku ule wa manane akatufukuza nyumbani.
Ha ha haa,ila mama wewe ni jasiri sana.

Binti yule alicheka kidogo kwenye maongezi yake kabla ajaendelea kusema na mwili wa mama yake ambao mapigo ya moyo yalikuwa yanadunda kwa taratibu sana kwa jinsi ile sauti iliyotoka kwenye mashine ya mapigo ya moyo pale hospitali ilivyokuwa inaonesha.

*********

Unajua kwa nini nimecheka? Nimekumbka usiku ule kabla hatujafukuzwa pale nyumbani. Ulimkunja baba shati lake, na alipoanza kukuletea matusi ulimchapa vibao kama mtoto mdogo. Japo nilikuwa nagugumia maumivu kwa lile teke alilonipiga baba, ila nilishuhudia ukitoa adhabu ile bila kujali yule ni mwanaume na ni mume wako,tena ni kichwa cha familia.

Sikusifu kwa kumpiga, heshima yangu kwake itabaki kama baba. Ila nakusifu kwa kunitetea hasa baada ya mimi kuja kukutea wewe. Japo nilikuwa sina uwezo wa kumfanya baba chochote,lakini nilikupa mwangaza kiasi chake ni nini ulipaswa kufanya baada ya kuona mimi napigwa kwa sababu nakutetea.

Maneno mazito yaliendelea kutoka mdomoni mwa binti yule na wakati huo yule muuguzi mkuu ni kama alivutwa sana na ile historia ya uchungu kutoka kwa mwana kwenda kwa mama.

Baba alikuwa amelewa na ndio maana uliweza hata kumpiga mitama na akasaliti amri, lakini kama angekuwa hajalewa siku ile ningeshuhudia mpambano wa ajabu sana, na katika kuepuka hilo ili lisije kutokea, uliamua kunichukua usiku uleule huku matusi ya baba yakitufuata,tukaondoka pale nyumbani. Kila kilichokuwa chetu kwa usiku ule,baba alishiriki kuturushia kwa kuwa alikuwa anavimiliki yeye katika chumba chake.

Tuliondoka pale huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha bila kukoma wala kupumzika. Ilikuwa ni mvua hasa. Mvua ambayo iliishia mwilini mwetu.

Bonyeza iyo Button Hapo Chini Iliyo andikwa Next Kutaza Sehemu inayo Fuata ya Simulizi Hii Amka Mama.

Written by Aisha Mapepe

Aisha Mapepe ni Mwandishi wa Simulizi Mbalimbali za Mapenzi, Maisha na za Kuelimisha. Lengo ni Kuburudisha Jamii na Kuondoa Stress za Maisha zinazo tukabili Baadhi Yetu.

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Akufukuzaye Akwambii Toka

AKUFUKUZAYE AKWAMBII TOKA: ASHURA NA BATULI

Sarafina Simulizi

SARAFINA: MOJA KATI YA SIMULUIZI PENDWA MNO