in

AMKA MAMA: SIMULIZI YA KUSISIMUA NA KUHUZUNISHA

*********

Sikujua tunaenda wapi lakini safari yetu iligotea mbele ya nyumba moja kubwa. Nyumba ambayo sikuweza kuitambua hadi pale tulipofunguliwa na mwenye nyumba ambaye kwa haraka niligundua ndiye mwenyekiti wa ule mtaa.

Hakutaka tuisogelee nyumba yake hata tusimame pale ambapo hapakuwa na mvua. Kwa kuwa yeye alikuwa na mwamvuli, basi hali ya kulowa kwetu yeye hakuitambua maumivu yake. Namkumbuka yule mzee, namkumbuka vizuri sana.

Sijasahau sura yake, sauti yake kali iliyotufukuza kwake na wala sijasahau jina lake maarufu pale mtaani, aliitwa Mzee Michanga. Binti alipofika pale alimeza mate ya uchungu kisha akaendelea kuelezea kilichotokea.

Yule Mzee Michanga ujue niliona kama utani pale alipotukatalia kwenda kusimama pale kibarazani ambapo tungejikinga na mvua na kumuelezea shida yetu. Ilikuwa kama utani kweli na mimi nilidhani anatania kwa jinsi mzee yule alivyokuwa ananipenda na kunitania japo nilikuwa sipajui kwake.
Ila nilishangaa ule utani umemuisha wote,alitufukuza kama mbwa pale kwake.

Au siyo kama mbwa, alikuwa anatufukuza kwa kutusukuma kama wafanyavyo askari waliomkamata kibaka ambaye anagoma kwenda kituoni.

*********

Yule mzee alitutoa nje huku bado mvua na baridi vikiendelea kutusakama miili yetu kana kwamba vilitumwa kwa ajili hiyo, na mvua ya Sumbawanga pamoja na baridi yake,siku ile ningesipobanwa na pumu, ningesipoumwa tena na na gonjwa lile. Ugonjwa ambao umetibika baada ya mimi kufanikiwa kimaisha, juzi tu hapa ndio nimetibiwa baada ya mume wangu kunipeleka hospitali moja kule Uholanzi.

Hizi ni taarifa nzuri kwako mama,najua huwezi kuamini hasa ukiikumbuka siku ile. Binti yule wa miaka ishirini na nane aliongea hayo kwa faraja huku akishika nywele za mama yake na muda mwingine kuzilaza.

Bado yule daktari alikuwa kaegemea katika mlango huku akiwa makini kufatilia yale maneno ya yule mwanadada. Dada ambaye kimuonekano ni kama alikuwa hajapitia yale maswahibu yale. Alikuwa ni nadhifu pamoja na kujiweka kama wasichana wa kileo.

Daktari akawa anaendelea kuyaingiza akilini maneno yaliyojaa uchungu mkubwa toka kwa mwanadada yule.

Tulifukuzwa pale,usiku uleule na mvua ikiwa inanyesha. Ulininyanyua na kunibeba kisha ukaanza kukimbia kulekea palipo salama,na wakati huo huku nyuma yule Mzee alibamiza geti lake na kuingia ndani.

Safari yetu iliishia kwenye kibanda kimoja cha makuti kilichopo pale mtaani kwetu, kibanda ambacho kiliponipokea,nikaanza kuumwa palepale.

*********

Kifua changu kikaanza kunibana bila kunipa nafasi ya mimi kupumua. Licha ya mengi yaliyotukia nyuma, ila pale ndipo nilidhihirisha kuwa uchungu wa mwana, aujuaye ni mzazi. Mwanadada aliinamia godoro la hospitali na kutoa chozi la uchungu lakini alipoamka hakuacha kuendelea kuongea alichokusudia.

Nikiwa na umri ule wa miaka saba ndani ya kibanda kile kidogo cha makuti tena mvua na radi zikizidi kupamba moto huku nje, kifua kile kilichosababishwa na pumu, kilinifanyaa ndani ya sekunde kumi nitoe pumzi moja tu!

Nilikuwa sijielewi, ni kama nilipoteza fahamu lakini bado nilikuwa nauwezo wa kusikia na kuona,lakini akili ililala kabisa. Najua mama ulihaha huko na huko kutafuta tiba lakini ulichoambulia ndicho kilichoniponya.Yale masarufeti uliyoyafanya kama kitanda changu, pamoja na zile nguo chache tulizotoka nazo nyumbani ambazo baadhi zililowa,ndizo zilikuwa mashuka yangu.

Hukuishia hapo mama,kwa upendo wako na uchungu juu yangu, ulitoa gauni lako ulilokuwa umelivaa ili ukinigusana nalo nisisikie baridi kwa kuwa lililowana. Ukalitupa pembeni na kunikumbatia ili uongeze joto katika mwili wangu,nani kama wewe mama? Ni nani kama wewe? Amka mama, tafadhali amka.

*********

Dada yule aliongea kwa uchungu uliojikita moyoni mwake hadi ule mwili wa mama yake ambao ulikuwa haujawahi kutikisika kwa miezi mitano mfululizo, safari hii ulitikisika.
Naam,kidole chake cha shahada kilitikisika na hata daktari mkuu aliona lile. Maneno ya mtoto yalimuingia mama,sasa akawa anapigana japo aweze kumuangalia mwanaye aliyeteseka naye kwa nusu ya maisha yake.

Daktari alitoka pale mlamgoni na kumfuata yule mwanadada na kumshika begani.
Binti endelea. Mama anapigania nafsi yake ili akuone. Endelea ulichokianza, usilie sana mwanangu. Daktari yule wa miaka kama sitini, alimfariji dada yule.

Dokta, hivi wajua ndugu yako wa kweli ni yule ambaye mmechangia damu ya wazazi na si yule uliyeunganika naye kutokana na mke au mume wako kuwa pamoja? Hapa na maana kwamba,ndugu wa mke wako si ndugu zako wewe. Kama uamini, basi subiri mkeo aondoke duniani uone kama watakuthamini hasa pale ambapo utakuwa huna kitu.

Sisemi haya kama nakutisha au kukukanya au kukujaza fikra zangu,bali nasema haya kwa kuwa nimepitia maisha haya,na nimeona kwa wenzangu pia wakiyapitia. Kwa hiyo namaanisha kwa ninachokisema. Mwanadada yule alimgeukia daktari mkuu wa hospitali ile na kumwambia maneno haya ambayo kwa daktari yawezekana yalikuwa mapya au yalikuwa kama nyongeza katika kujifunza kwake.

Mama yangu ujue alitolewa na wale wanandugu nje ya chumba kile kilichohifadhiwa maiti na kuambiwa yeye ndiye kamroga baba. Na vile vidole ambavyo vilikuwa vinatulenga wakati tumefika pale,vilikuwa vinatulenga kwa ubaya.

*********

Nasema vilitulenga kwa ubaya kwani pale mama alipobwagwa nje na wale ndugu wa baba, mara vidole vile viligeuka na kuwa midomo.
Wale waliyotuoneshea vidole, wakasimama kishughuli zaidi.Kila neno chafu ambalo waliona sawa kulitupia kwenye himaya ya mama yangu, walilitupia bila kumuonea huruma. Ni kama walishajazwa ujinga wale watu wa kule. Waliamini mambo ya kishirikina kuliko MUNGU, Sijui ni watu wa aina gani na sijui wataelimika lini.

Wanavyosema eti walienda kwa mganga ndipo yule mganga akasema mama yangu ni mchawi na ndiye kamroga mume wake kwa kuwa baba alitufukuza pale nyumbani. Hivi kweli hata wewe dokta waweza kuamini hilo? Waweza kukubali kuwa mama yako ni mchawi na wakati kaishi mumewe miaka kumi na mitano bila mumewe kutoa maneno hayo.

Kweli kabisa,waweza kuamini hilo dokta? Maneno yanayoweza kumtoa yeyote machozi yaliendelea kutolewa na dada yule mrembo.

Dokta alikuwa mtu wa kutikisa kichwa kushoto na kulia kama mwenye kusikitikia yale ambayo yalikuwa yanamtoka binti wa miaka ishirini na nane. Binti ambaye alikuwa sawa kabisa na binti wake wa pili.

“Nyamaza mwanangu. Hayo yote ni mapito tu! Sidhani kama nikikwambia hakuna marefu yasiyo na ncha, utakataa usemi huu kwa kuwa sasa ulishavuka hayo yote. Kinachokuangalia kwa sasa ni uhai wa mama yako.

*********

Ni wewe uliyeweza kufanya kiungo chake kimoja kitikisike, naamini ni wewe pia ndiye utafanya hata mdomo wake uongee,macho afumbue na mwili wake usimame wima kwa ajili ya kuendeleza mapambano ya maisha haya. Daktari aliongea kiushauri zaidi na kumfanya yule dada amuangalie mama yake pale kitandani akihemea mipira.

Mama Hakuwa Hivi, Hukuwa mtu wa kuhemea mipira kama gari au mashine ya kunyonyea mafuta. Hukuwa hivi mama. hukuwa hivi kabisa. Hukuwa mtu wa kulala muda mrefu hivi bila kusema chochote.

Sikuwahi kukuona umeamka saa moja asubuhi bali muda wako ulikuwa ni saa kumi na moja au saa kumi mbili. Yote hayo uliyafanya ili kuhakikisha unatafuta chochote kwa ajili ya maisha yetu. Na ulifanikiwa hilo mama yangu.

Hata siku ile nilipobanwa na pumu usiku,hukuweza kulala kwa raha na hata ulipolala sidhani kama ulikuwa unaota kitu kingine zaidi ya maisha yangu. Sijui nikufananishe na nani,wewe ni mama wa aina gani? Ni mwadamu gani wewe mama?

Ni mwanadamu gani ambaye anaweza kufurahi nilipodai chakula baada ya usiku ule wa ugonjwa wangu kupita? Nilidai chakula mimi kana kwamba pale nilikuwa nyumbani na kumbe tulikuwa kwenye kibanda kilichotuhifadhi kwa muda tu!

*********

Lakini wewe hukujali hilo. Nilipokuamsha kwa sauti chovu na kukwambia nahisi njaa. Wewe ulitabasamu na kunikumbatia huku ukilia na kuniambia ulidhani nitakuacha mpweke.
Nisingeweza kukuacha mama yangu. Naomba na wewe usiniache. Amka mama, tafadhali amka. Safari hii wakati dada yule anaongea, chozi lilimtoka yule mama kwenye jicho lake la upande wa kushoto.

Ama hakika ilikuwa ni muujiza,hata daktari alishindwa kuvumilia na akajikuta akitoa chozi baada ya kuona mama yule anatoa chozi ambalo hakuwahi kufikiria kama itakuja kutokea kwa kitu kama kile. Mama yule alikaa kwa muda mrefu sana pale hospitali, hiyo ndio sababu ya hata daktari kutoa chozi lake ambalo naweza kusema lilikuwa ni la furaha.

Kila mara ulitoa chozi kwa sababu yangu. Naamini hata sasa unafanya sawa na kile nachokiamiani. Umetoa chozi kwa sababu una uendo juu yangu. Nami nakupenda sana mama, ila nakuomba uamke ili nikuoneshe upendo huo. Huruma na huzuni iliendelea kutawala ndani ya chumba kile cha wagonjwa walio mahututi kutokana na maneno aliyoyatoa binti yule.

Ulitoa chozi la uchungu pale ndugu wa baba walipokupora na kunichukua mimi ili niishi nao kwa kusema eti mimi nilikuwa damu ya baba na si yako. Ulinililia sana nakumbuka. Sikuwa nyuma kulia pia, nilikulilia huku nanyoosha mkono unikamate,lakini haikuwezekana. Walikuwa wamekamata vizuri tayari kwa kunipeleka ndani na kunifungia huko.

Nachojua walikufukuza pale msibani na hata kwenye mazishi hawakutaka kukuona kwa ahadi ya kuwa kama ungeenda, wangekumaliza. Mate mazito na ya uchungu yalipita kooni kwa dada yule kabla hajaendelea kuongea aliyoyaanza.

*********

Baada ya mazishi ya baba. maisha yalianza upya. Mimi nikiwa nalelewa na mama wa kambo na pale nyumbani akiwepo baba mdogo tukiishi naye.Hiyo ni baada ya kukaa kikao cha familia, maamuzi yao yalikuwa hivyo. Hawakukuzungumzia wewe hata kidogo.

Nashukuru baba mdogo alikuwa ananijali sana. Shule alinianzisha na kila nilichokiomba alinipatia. Ila tatizo lilikuwa kwa huyu mama yangu wa kambo. Huyu ndiye chanzo cha mimi kujua kuwa baba aliwekewa sumu katika chakula, na ni huyu huyu ambaye alitaka kuniua na mimi na ndio maana nilikutafuta usiku na mchana ili nirudi kuishi na wewe.

Nisingeweza kukaa na yule mama muuaji. Dada yule aliendelea kuongea kwa masikitiko huku sauti yake ikijaa kilio kikubwa ambacho ni MUNGU pekee ndiye awezaye kupima ni kiasi gani kilikuwa kina maumvu.

Bonyeza iyo Button Hapo Chini Iliyo andikwa Next Kutaza Sehemu inayo Fuata ya Simulizi Hii Amka Mama.

Written by Aisha Mapepe

Aisha Mapepe ni Mwandishi wa Simulizi Mbalimbali za Mapenzi, Maisha na za Kuelimisha. Lengo ni Kuburudisha Jamii na Kuondoa Stress za Maisha zinazo tukabili Baadhi Yetu.

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Akufukuzaye Akwambii Toka

AKUFUKUZAYE AKWAMBII TOKA: ASHURA NA BATULI

Sarafina Simulizi

SARAFINA: MOJA KATI YA SIMULUIZI PENDWA MNO