I Will be Back: Sehemu Ya Tano (5) Mwisho
Pia wenzetu walijali sana muda mkikubaliana kitu fulani ni saa moja kamili basi kweli ni saa moja kamili hakuna samahani au bahati mbaya za kipumbavu kwa wenzetu.
Ndani siku mbili ndege ya abiria Air bus C283 ilitua Mombasa. Bendera ya Marekani na chapa zote za ndege zilitoka zimefutwa hukohuko Marekani ili kuficha utambulisho wa ndege hio. Jambo lingine lililofanya tutumie ndege binafsi ilikua kukwepa usumbufu wa kukaguliwa mizigo uwanjani.
Bila kupoteza muda tulipakia mizigo yetu, silaha, ma begi pamoja nyenzo zote zilizohitajika kwenye ile mission.
Air bus C283 ilikua na uwezo wa kubeba abiria 290 lakini umuhimu wa ile mission ulifanya watu 40 pekee tujiachie ndani yake tena bure kabisa.
Air bus C283 iliiacha ardhi ya Mombasa ikakata mawingu kwa masaa kadhaa kisha tukaenda kutua uwanja wa ndege wa kijeshi uliopo Ukonga banana jijiji Dar es salaam.
Tulivyotua tu James alienda ofisi za jeshi uwanjani hapo, aka saini nyaraka kadhaa kisha akatumia simu ya ofisi hiyo kuongea na balozi wa Marekani nchini Tanzania. Haikupita muda magari kumi aina ya V8 yalikuja pale uwanjani yakatubeba sisi na mizigo yetu yote mpaka ofisi za balozi wa Marekani nchini Tanzania.
Ubalozini tulipewa chumba kilichokua na kila kitu kama ilivyokua ile nyumba ya maajabu kule msituni Nakuru.
Hatukua na muda wa kupumzika tulivyoingia ndani ya kile chumba balozi wa Marekani aliingia kuongea na sisi, alitusisitiza sana kufanya juu chini kuhakikisha Abrahamu Odhiambo anakamatwa akiwa hai au amekufa.
Baada ya maongezi alipiga video call kwa boss wake, raisi wa Marekani ambaye aliongea uso kwa uso na James huku na sisi tukishuhudia live.
“James you and your team you are doing this on behalf of American people if possible take him alive otherwise shoot him down” (James wewe na timu yako mnafanya hivi kwa niaba ya watu wa Marekani kama ikiwezekana mkamateni akiwa hai ikishindikana mmue) rais alisikika kupitia video call.
“Yes Mr. President I promise we will bring him alive” (Ndio Mr. President naahidi tutamleta akiwa hai)
“Thanks for your service. God bless you all God America” (Asante kwa huduma yenu. Mungu awabariki wote Mungu aibariki Marekani) Raisi alisema akapiga saluti nasi tukampigia kisha video call ikakata.
Kila kilichofanyika kiliniongezea motisha, kwangu kupigiwa na kumpigia saluti raisi wa Marekani au raisi wa dunia kwa uhalisia uliofichika lilikua jambo muhimu sana kwangu, nilijisikia fahari kuna kitu fulani kisichoelezeka kiliuvaa mwili wangu nikajiona nimekua mwepesi.
Simu ilivyokatika balozi alirudi ofisini kwake bila kupoteza muda James alisogea mbele zaidi.
“1:00 am today we will start our mission we will go to Mr. Davis house and catch all bastard they will help us to find Abraham Odhiambo” (Saa 7 kamili usiku wa leo tutaanza mission yetu tutaenda nyumbani kwa Mr. Davis na kuwakamata wanaharamu wote watakao tusaidia kumpata Abraham Odhiambo)
James alituambia kisha afungua ramani ya nyumba yangu kwenye ile smart tv tuliyoitumia kuongea na raisi muda mfupi uliopita. Nikiwa katika kujiuliza mahali alipoitoa hio ramani James akaanza kutuelekeza jinsi tutakavyoingia ndani ya nyumba yangu, tutakavyowatia nguvuni wafanyakazi na jinsi ya kutoka nje.
Alipomaliza alifungua ramani nyingine ya msitu wa Magopande. Safari hii aliomba tumsikilize kwa makini zaidi alisisitiza lazima kila mtu aelewe kile alichokua anaenda kukiongea.
James alituonyesha ile ramani kwa kutumia pointer ya rimoti.
Ulikua msitu wa Magopande mahali aliposadikika kuwepo Abraham Odhiambo pamoja na kundi lake lote la uhalifu.
Kupitia ile ramani James alituelekeza jinsi ya kuingis ndani ya ule msitu, jinsi tutakavyo wakabiri wapiganaji wa Odhiambo. James alitusisitiza kua makini kuhakikisha tunamkamata Odhiambo akiwa mzima huku akituonya kua uzembe wowote unaweza kuyagharimu maisha yetu.
Kila tukio lilipangwa namna ya kufanyika kwa jinsi mambo yalivyopangiliwa hata kabla ya mapigano mtu ulikua ushaanza kusikia harufu ya ushindi.
Baada ya maelezo yote, James aliniita pembeni mimi Joel na Slyvester, alitupa maelekezo yetu binafsi kua tutakapoivamia nyumba yangu sisi hatutaingia ndani kwangu bali tutamvamia Mzee Ambrosi na kumzimisha kwa dawa ya usingizi ili tutumie nyumba yake kupata shabaha nzuri za ki sniper wakati tukifanya back up.
Baada ya maelekezo yote kumalizika yule mzungu wa kike niliedhani ni mpenzi wake na Joel hapo awali alifungua mabegi na kumkabidhi kila mtu nguo za kuvaa wakati wa mission, alitupa dakika 20 kila mtu awe amezivaa ili aturuhusu kwenda kwenye chumba cha silaha.
Dakika kumi na tano zilimtosha kila mmoja kuvaa zile nguo bila kupoteza muda tukaenda chumba cha silaha tulichokikuta humo hakielezeki kulikua na bunduki za kila aina, bastola, smg, sniper guns, mabomu ya machozi na ya kutupa kwa mkono, makombora tu ndio sikuyaona nadhani waliogopa kuwatisha Watanzania.
Saa saba kamili usiku ilifika. Tukiwa ndani ya mavazi maalumu ya kazi timu yetu nzima ya watu arobaini tuliianza mission yetu, tulitumia yale yake magari kwenda nyumbani kwangu maeneo ya mbezi beach.
Tulipokaribia kufika tulishuka tukapaki magari mbali mbali kwenye giza ili kuogopa kushtukiwa.
James aliiongoza timu nzima alitugawanyisha makundi matatu, kundi langu nilikua mimi, Joel na Slyvester kazi yetu ilikua kuvamia nyumba ya jirani yangu Mzee Ambrosi na kumzimisha ili tuweze kuitumia nyumba yake kupata shabaha nzuri.
Kwa kua tulikua watu w kutoa back up (msaada) kundi letu lilianza kutekeleza majukumu wengine waliizingira nyumba yangu lakini hawakufanya kitu walisubiri mpaka tukamilishe kazi yetu.
Kwa umakini mkubwa na kunyata kwa kujificha, mimi, Joel na Slyvester tulilifikia geti la Mzee Ambrosi. Ilikua usiku sana kupiga hodi kungewashtua wale wahalifu na Mzee Ambrosi mwenyewe, ili kuepusha kelele nilimpigia simu Mzee Ambrosi baada ya dakika kadhaa alipokea, nilimuomba radhi na kumuomba aje anifungulie geti maana nilikua nje.
Wema wake ulimponza Mzee Ambrosu alipofungua geti Joel alimziba pua zake na kitambaa chenye dawa ya usingizi bila ubishi Mzee Ambrosi alilala, tuliingia ndani tulifunga geti tukamkokota Mzee Ambrosi na kwenda kumlaza chumbani kwake. Msako mdogo ulifanyika tukawapata watu wanne, dada wa kazi na wanaume watatu nao bila kupoteza muda Joel akawazimisha na ile dawa ya usingizi.
Tulienda chumba kikubwa cha ghorofa ya juu, Joel alitumia kifaa maalumu kukata pazia na kioo cha dirisha usawa wa mdomo wa bunduki, alifunga silencer ili kuzuia mlio wa risasi kisha akautoa mdomo wa bunduki kwenye lile tundu dirishani. Kazi yetu ilikua tayari, Joel alimpa ishara Sylvester bila kuchelewa microphone ndogo sikioni kwa Slyvester ilifanya kazi yake.
“We are in position” (Tupo eneo husika) alimwambia James.
Giza lilikua kubwa kupita kawaida wale wahalifu walikua na akili sana walibadilisha taa zote za nje na uani wakaweka taa za rangi zenye mwanga mdogo sana, ilihitaji umakini mkubwa sana kuweza kuwaona. Tulikua dirishani kwa Mzee Ambrosi jengo la juu kazi yetu ilikua tayari Slyvester alimjulisha James kua tayari tupo eneo husika.
“There is any people outside?” (kuna mtu yoyote nje) James aliuliza.
“Yes” (ndio)
“How many?”(wangapi)
Mwanga hafifu wa zile taa za rangi ulitupa shida kuweza kupata idadi kamili ya watu. Joel alinipa darubini ndogo kisha naye kwa umakini mkubwa alitumia lenzi ya bunduki yake, wote kwa pamoja tukaanza kuwahesabu.
“There is nine people” (kuna watu tisa)
“Are you sure?” (mna uhakika)
“Yes” (ndio)
“Ok take them down” (sawa wauweni) James alitoa amri.
Kulikua na watu tisa wenye bunduki walioizingira nyumba yangu nzima ndani ya ua ili kuipa ulinzi. Kona zote nne za ua zilikua na mtu mmoja mmoja, getini walikuwepo wawili, mlango wa nyuma nyumba kubwa walikuwepo wawili, mlango wa mbele wawili na mlango wa stoo ya nje alikuepo mmoja, idadi ya watu tisa ilitimia.
Amri ya James kwa Joel ilikua ni kama kuangua maembe, wazungu walituletea dini ya kikristu yenye amri ya kukataza kuua lakini kilichotokea hapo utasema dini haikutoka kwao.
Dakika mbili zilikua nyingi, ndani ya dakika moja miili ya watu wote tisa ilikua chini na bunduki zao.
“Clear” (safi) Slyvester alitoa taarifa.
“Good job” (kazi nzuri) James alijibu.
Bila kupoteza muda ile timu ya watu wetu waliokua wameizingira nyumba yangu nje waliingia ndani kwa kuruka ukuta walikua na uwezo wa kuvunja geti lakini waliogopa kuwashtua maadui waliopo ndani kwa sababu hatukujua idadi yao kamili na aina za silaha walizokua nazo.
Muda wote huo kidole cha Joel kilikua bado kwenye kitufe cha kufyatulia risasi kuhakikisha hakuna adui atakae leta changamoto yoyote.
Kwa umakini mkubwa timu yetu nzima iliingia ndani ya nyumba yangu kubwa. Kazi yetu kubwa sisi ilikua ni kuhakikisha hakuna adui yoyote atakayetoka nje na kukimbia.
Haikupita muda toka waingie ndani tukaona baadhi ya wahalifu wa yule mwanaharamu wakikimbia kutoka nje. Joel alifanya kazi yake, alikua ni kama anakunywa juisi ya matunda. Aliwafyatulia risasi wale maadui bila kumkosa hata mmoja, hakuna aliyepona wote walianguka chini na kufa kama kuku.
Milio ya risasi ilisikika ndani ya nyumba yangu kubwa kutoka kwenye bunduki za wale wahalifu ambazo hazikua na viwambo vya kuzuia milio ya risasi.
Muda wa dakika saba hadi nane ulipita ghafla milio ya risasi ya bunduki za wale wahalifu wa Ambraham Odhiambo iliacha kusikika.
Hakujua nini kimetokea, pale dirishani mimi, Joel na Sylvester tulibaki njia panda, hatukujua ni nani aliyemtia nguvuni mwenzake, timu yetu ama wale wahalifu wa Odhiambo.
Tulisubiri dakika tano nzima lakini wapi, ukimya mkubwa ulitawala, hakukua na mtu hata mmoja aliyetoka nje, si wa timu yetu wala wa Odhiambo. Nini kinaendelea? wote tulijiuliza swali moja lililokosa jibu.
Hofu kubwa ilianza kututafuna ikasindikizwa na jasho jembamba lililo mlowanisha kila mmoja.
Sylvester aliamua kumpigia simu James kumuuliza nini kinaendelea. Lakini ghafla! hata kabla hajakaa sawa simu ya James iliingia.
“We have them” (tumewakamata)
“Woooooh!!” tulishangilia.
Kazi ya kwanza ilikua imemalizika, tulitoka pale dirishani na kwenda kuungana na wakina James nyumbani kwangu. Mzee Ambrosi na wale ndugu zake wanne tuliwaacha kama walivyo, dawa tuliyoitumia haikua na madhara yoyote hivyo wangeamka wazima wa afya pindi ambapo ingeisha nguvu.
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne nilitia miguu ndani ya nyumba yangu.
Niliingia ndani vyumba vyote hakukua na cha kujivunia kila kitu kilikua hovyo hovyo, matundu ya risasi ukutani, maiti na damu vilitapakaa kila kona ilikua ni kama nimeingia kwenye machinjio ya wanyama.
Wahalifu 22 walikamatwa wakiwa hai mikono yao yote ilifungwa pingu kusubiri kifuatacho itv. Tressy na Motemapembe hawakuwepo hii iliashiria kua bado tuna kazi kubwa ya kufanya hapo mbele kuhakikisha mwanaharamu huyo anakamatwa kwa njia yoyote ile.
Wote pamoja tulikusanya maiti za wahalifu waliouwawa wakati wa kurushiana risasi.
Tulipata maiti kumi na tisa, maiti tisa zilizouwawa na Joel pale uani hazikuharibika sana kama zile tulizozitoa ndani kwa sababu Joel alitumia kila risasi moja maiti moja.
Kila kitu kilikua kimepangwa toka awali hivyo ile miili haikutupa shida, James alipiga simu ubalozini kwao, mawasiliano yalifanyika haikupita muda polisi wa Tanzania walikuja kuchukua zile maiti, uchunguzi na kila kitu tuliwaachia wao, sisi tuliwabeba wale wahalifu 22 tukaondoka nao kwenda ubalozini.
Ilikua saa tisa na nusu usiku tulitumia karibu masaa mawili na nusu kukamilisha kila kitu. Ubalozini balozi alitupokea kwa furaha, alitupongeza kufanikiwa kuwakamata wale wahalifu bila hata mtu wetu mmoja kujeruhiwa kisha akatupisha tufanye kazi yetu.
Tulitumia chumba tulichopewa na balozi hapo awali. Ndani ya chumba hicho kulikua na chumba kingine ambacho sikua nimekiona awali. Tuliwapeleka wahalifu wote 22 humo ndani kufanya mahojiano yatakayo tusaidia kupata sehemu ya kuanzia kumtafuta Ambraham Odhiambo.
Chumba cha mahojiano tulipokelewa na kila aina ya kifaa cha mateso unachokifahamu wewe. Mwili ulisisimka, kama ningeambiwa nikipe jina kile chumba ningekiita chumba cha mauaji sababu kilitisha kuliko hata wodi za upasuaji au machinjio ya wanyama.
Mahojiano mazito yalifanyika mle ndani, James aliwauliza maswali mimi nikayatafsiri kwa kiswahili. Niliwaonea huruma sana wale wahalifu niliwaonya mapema kitakachotokea kama hawatajibu maswali au watadanganya, kwa bahati mbaya hawakunisikia.
Muda wa kuchekeana na kubembelezana haukuwepo. Meza kubwa ilisogezwa mbele, vifaa vyote vya mateso viliwekwa juu yake. Kilichofuata hapo na zaidi ya kile nilicho kishuhudia kwenye filamu za kimagharibi
Wale wahalifu waliteswa, wa kupigwa ngumi alipigwa, wa kung’olewa jino aling’olewa, mwenye kupigwa shoti ya umeme alipigwa. Ndani ya nusu saa sura zao hazikutamanika zilikua kama chapati zilizokosa mafuta, ilikua afadhali kwa wale waliofariki maana walikua wamepumzika kuliko walichokipata wao muda huo.
Mateso yalizidi, uvumilivu uliwashinda mwisho wa siku walisema kila kitu walichokifahamu kuhusu Abraham Odhiambo.
Taarifa zote muhimu tulizozihitaji tulizipata kilichobaki ilikua kuzifanyia utekelezaji. James alitupa muda wa kupumzika, alituambia kesho yake saa sita usiku kazi ya kwenda kumkamata Abraham Odhiambo itaanza. Sekunde zilienda, dakika zikakatika hatimaye muda wa ile kazi yetu nzito ulifika.
Ilikua saa sita kamili usiku kila mtu alikua tayari ndani ya nguo za kazi. Safari ya kwenda msitu wa magopande ilianza. Ukimya mkubwa ulitawala, kwangu hofu ilikua kubwa kuliko mtu yoyote mle ndani, sikua mzoefu kama wenzangu, njia nzima zima nilisali kumuomba Mungu.
Tulifika msituni magopande, safari hii tulitumia gari moja min bus ndogo. Giza kubwa lilitusaidia hatukuhitaji kulificha kama safari ya kwanza. Tuligawanyika makundi matano ya watu nane tukasambaa kuzunguka msitu mzima kisha safari ya kuingia katikati ya msitu ikaanza.
Ndani ya dakika kadhaa makundi yote tulikutana mbele ya ukuta mrefu uliokua na geti kubwa mbele. Kulikua na walinzi sita wenye bunduki mikononi.
.
James, Joel na watu wengine wanne walitambaa chini ya majani marefu kusogea getini, walipokaribia waliwafyatulia risasi wale walinzi wote wakaanguka chini.
Walizificha maiti kwenye majani, walibebana kupanda ukuta wakaingia ndani. Haikupita muda geti lilifunguliwa wote tuliokua nje tukaingia ndani kimya kimya bila kumshtua mtu.
Ndani vitu viwili vilitusaidia sana cha kwanza viwambo vya kuzuia milio ya risasi vilifanya tuwaue maadui wengi bila kushtukiwa cha pili majani makubwa yalitusaidia kujificha vyema.
Tulikua wachache lakini tuliua maadui wengi haraka, ndani ya saa moja tulikua tumeua zaidi ya wahalifu mia tatu bila ya kujulikana.
Jambo hili lilitupa urahisi kuingia mahema mengi yaliyokuwepo humo ndani.
Kila hema tuliloingia hatukufanikiwa kumuona Tressy wala mwanaharamu Motemapembe. Tuliwaua wahalifu wengi zaidi ili tupate nafasi Kubwa ya kuingia mahema mengi.
Lakini karibu mahema yote hatukuambulia kitu. Tulimkamata mualifu mmoja, tulimuuliza mahali alipokuwepo kiongozi wao lakini hakusema.
James alimpiga risasi miguu yote miwili akili zilimkaa sawa akatuambia sehemu alipokuwepo Motemapembe. Alipomaliza tu, James alimpa moja ya kichwa akamuua, tulikua wachache sana kuanza kuhudumia majeruhi.
Tulitakiwa kumkamata Motemapembe usiku kabla hakujapambazuka hivyo yule mhalifu alivotuambia tu sehemu alipo tulienda moja kwa moja bila kupoteza muda.
Kila tuliyekutana nae mbele yetu tulimfyatulia risasi mpaka tunafika sehemu alipokuwepo Motemapembe. Tulikutana na walinzi nje kwa umakini mkubwa tukawakabili ndani ya dakika mbili miili yao ilikua chini.
Ilikua jumba kubwa la kisasa ambalo halikustahili kuwepo msituni.
Motemapembe alikua humo ndani, yale mahema waliyatumia wafanyakazi wake tu.
Tuliingia ndani tukapokelewa na korido refu lenye vyumba kila upande kwa haraka haraka vilikua zaidi ya vyumba 50.
Tuliingia chumba hadi chumba, kila tuliyemkuta tofauti na Motemapembe tulimfyatulia risasi tukamuua.
Tulimaliza karibu vyumba vyote bila kumuona Motemapembe, vyumba vitatu vilibaki, tuligawanyika makundi mawili kundi moja likaenda chumba cha kwanza, wengine wakaenda chumba cha pili, mimi peke yangu nikaenda chumba cha tatu baada ya kusikia sauti ya mziki ikitokea humo.
Niliamini lazima Tressy au Motemapembe mmoja wapo atakuepo humo.
Kihelehele flani hivi amazing kilinishika, nilitangulia mbele nikafungua mlango kwa tahadhari huku nikiwa nimejiandaa kufyatua risasi. Kuingia ndani sikuamini nilichikiona, nilikutana uso kwa uso na Tressy. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne tukaonana tena ana kwa ana.
“Tressy ni wewe?” sikuamini nilipomuona.
Hasira zilinishika, hata kabla Tressy ajanijibu neno lolote nilimuwekea bunduki kichwani, kumuona kulizidi kuniumiza.
“Sali sala yako ya mwisho” nilimwambia.
Tressy alianza kucheka, maneno yangu ya kumwambia asali sala ya mwisho yalimuingia sikio la kulia na kutokea la kushoto, labda alidhani namtania lakini mimi sikua na masihara hata kidogo, niliona kama ananichelewesha.
“Moja.. Mbili.. Taaaaat..u” ile nataka kufyatua risasi nikasikia sauti.
“Stop you shoot I shoot” (acha ukifyatua, nafyatua)
Kama Tressy alivyodhani namtania mimi pia nilidhani ile sauti inanitania, suala la kushusha bunduki chini halikuniingia akilini, sikushusha bunduki chini. Ile sauti haikujua kubembeleza, nikiwa bado nimeshikilia bunduki niligeuka ili kumtazama aliyeniambia yale maneno lakini hata kabla sijamuona sura nilipokelewa na kitako cha bunduki usoni, ndani ya sekunde moja niliona giza zito mbele yangu nikaanguka chini nikapoteza fahamu.
Nilikuja kushtuka na kujikuta juu ya kitanda kidogo cha chuma ndani ya chumba chenye ukubwa wa wastani. Uso wangu ulikua umeshindiliwa na bandeji nzito lililonuka madawa ya kila aina. Mwili wote ulikua unauma, kichwa kilikua kizito kama tikiti maji. Ukungu mkubwa ulikua umetanda machoni kwangu, nilishindwa hata kuiona vizuri mishale ya saa kubwa iliyokua imetundikwa ukutani karibu kabisa na kitanda nilichokua nimekilalia.
Harufu za madawa kwenye ile bandeji zilinipa majibu kua nilikua hospitali.
Kwanini nipo hapa? Nilijiuliza lakini sikupata majibu. Nilijaribu kuvuta kumbukumbu nini kilichotokea lakini sikukumbuka kitu.
Kitendo cha kushindwa kukumbuka kilichotokea kilafanya niangaze macho yangu mle ndani ili nipate mtu wa kuniambia chochote. Macho yangu yalikua mazito kwa sababu ya ukungu lakini niliweza kutambua sura za watu wote niliowaona mle ndani.
Nilitazama kwa makini pande zote mle ndani, sikutaka kuamini nilichokiona.
Macho yangu yalitua kwenye uso wa Tressy pamoja na mtoto, ilikua kama mazingaombwe, anafanya nini hapa? Lilikua swali lingine lililoniumiza kichwa.
Tressy na yule mtoto niliyemuacha wakati naenda kusoma walikua mbele ya kitanda changu pamoja na ile timu yangu nzima ya FBI ya watu arobaini. Tressy alikua huru kabisa, hakua na pingu wala kamba yoyote mikononi, kiukweli nilibaki njia panda, ilikua vigumu sana kufahamu na kuelewa nini kinaendelea.
Kumuona Tressy na yule mtoto kulinichefua sana, hasira kali zilinishika, amekuja kukudhihaki, akili yangu iliniambia.
Ghafla nilipata nguvu za ajabu, sikujali hali yangu maumivu yote ya mwili yaliisha.
Nilijikuta nikiruka kutoka pale juu ya kitanda na kwenda kumpamia Tressy, yule mtoto mdogo sikumgusa, sikuona kosa lake lolote.
“Lazima ufe Tressy,kwa sababu umeniumiza sana” nilisema kwa sauti.
Ghafla hata kabla sijamfikia James na Joel walinizuia. Walinikamata kwa nguvu, baada ya purukushani za hapa na pale walifanikiwa kunirudisha kitandani.
Baada ya kunirudisha kitandani, James kiongozi wa ile timu yetu alianza kuniambia mambo ambayo yalikua magumu sana kuingia akilini.
“Very sorry Davis put all blame on us” (pole sana Davis tulaumu sisi).
“What is going on?” (nini kinaendelea).
“Tressy is on our side and this kid is your son” (Tressy yupo upande wetu na huyu mtoto ni mwanao)
Niliacha mdomo wazi kwa mshangao mpaka udenda ukanitoka, maswali mfululizo yaligombaniana siti kichwani mwangu, lakini hata kabla sijaanza kuyapunguza kwa kwa kuuliza, James aliniwahi na kuendelea kuniambia.
Tressy alikua ni wakala wa kitengo cha FBI kinachohusika na kazi zote zinazofanyika nje ya nchi ya Marekani.
Sikua na la kufanya, nilikua mpole kama bundi mjane aliyedhurumiwa kiota, macho na masikio yangu yote yalikua kwa James, nilimsikiliza kwa makini.
Tressy hajakusaliti kama unavyodhani, James alizidi kuniambia.
Tressy alikua amejilengesha kwa mwanaharamu Motemapembe ili ampeleleze kiundani, sisi ndio tuliempa kazi hiyo kwa sababu tulihitaji habari za Motemapembe kuliko kitu kingine chochote.
Yeye ndiye alikua anatutumia kila kitu, habari, ripoti na mambo yote kuhusu Motemapembe, hata idadi ya wanajeshi na ramani ya msitu wa Magopande alitutumia yeye.
Mpaka wakati huu ninapoongea na wewe, tayari Motemapembe tushamkamata tunasubiri kumpeleka nyumbani kama nilivyomuahidi raisi kwa niaba ya timu nzima.
Tuliamua kukushirikisha katika mission yetu tokea mwanzo ingawa haukustahili lakini lengo letu lilikua ili ije kua rahisi kuyaamini maneno yetu ndio maana tulianza kukufuatilia toka ukiwa masomoni nchini China, James alizidi kusema.
Kisha akaniambia mwana timu mwenzetu ndiye aliyenipiga na kitako cha bunduki ili nisiweze kumuua Tressy kwa sababu alikua upande wetu.
Pia aliniambia kua hata yule mtoto ni wa kwangu na hakuepo kwa yule mwanaharamu kama nilivyodhani bali alikua nyumbani kwa wazazi wangu Morogoro, wao pia walikua wanajua kila kitu ndio maana hawakuja kunipokea wala hawakutaka kujua habari zangu kutoka nilipokua nasafiri kurudi Tanzania.
Yalikua maneno mazito mno hadi James anamaliza kuniambia huwezi kuamini pamoja na ukatili wa wale watu wa FBI wa kuwatesa na kuwaua watu kama kuku kila mtu alilia, Tressy na yule mtoto nao pia walilia ilikua uchungu wenye furaha.
Baada ya maelezo ya James niliamini kila kitu, kwa msaada wa kitambulisho cha Tressy cha FBI pamoja na majibu ya vipimo vya DNA waliyokua wamenifanyia bila mimi kujua wakati nikiwa nimepoteza fahamu, nilimsamehe Tressy kwa moyo wote.
Nilijiona mkosaji sana kutaka kumuua Tressy ambaye masikini ya Mungu alikua ananipenda kwa dhati bila mimi mwenyewe kujua.
Sikutaka kupoteza muda niliinuka kitandani kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne nilimkumbatia mke wangu Tressy.
Kwa furaha kubwa niliibusu midomo yake, tukabadilishana mate bila kumsahau mtoto wangu nilimuinua juu nikamkumbatia kwa furaha. Mvua kubwa ya makofu ilinyesha, timu nzima ya watu 40 walitupigia makofi mfululizo, kila mtu alifurahi.
Nilikua hospitali ya jeshi mchana huo niliruhusiwa kutoka mimi na timu yetu tukaenda ubalozini, kwa macho yangu nilimuona Motemapembe akiwa amefungwa pingu mikononi na miguuni ndani ya jela ndogo.
Usiku timu tulipata chakula cha pamoja na wafanyakazi wote wa hapo ubalozini wakiongozwa na balozi. Kesho yake asubuhi tuliisindikiza ile timu yetu uwanja wa ndege wa jeshi Banana Ukonga, wakaondoka na ile ile ndege iliyotuleta kutoka Mombasa wakiwa pamoja na muhalifu wao, Abrahamu Odhiambo maarufu kama Motemapembe.
Mimi na familia yangu tulienda kukaa hotelini kupisha ukarabati wa nyumba yangu kuondoa mashimo ya risasi.
Baada ya wiki moja ilikamilika tukarudi nyumbani, siku hiyo hiyo tulienda kwa Mzee Ambrosi nikaomba radhi kila kitu kilichotokea, kwa kutumia pesa tulizopewa ubalozini tulilitengeneza lile dirisha la Mzee Ambrosi na kumnunulia mapazia mapya.
Nyumbani kwangu tulifurahi sana wote tulicheza kama watoto.
Usiku ulipofika kwa mara ya kwanza tena baada ya miaka minne iliyopita nilizama kwenye ulimwengu wa huba, nilifanya tendo la ndoa na mke wangu Tressy, baada ya tabu nyingi hatimaye furaha ikawa upande wangu.
Baada ya mwezi mmoja tulipokea mualiko kutoka nchini Marekani kwenda kuishuhudia kesi ya Motemapembe. Kabla ya kuondoka tulienda Morogoro nikawasalimu wazazi wangu kwa furaha kubwa tukafanya sherehe ndogo kupongezana.
Nilienda na Tressy na mtoto wetu mpaka nchini Marekani.
Siku ya hukumu ilifika, Motemapembe alihukumiwa kunyongwa baada ya mateso mengi aliyokua ameyapata.
Baada ya kesi raisi alitupa mualiko white house, alitushukuru kwa kila kitu kisha akatupa hati ya kuishi Marekani pamoja na nyumba iliyokua na kila kitu kama shukrani ya yale tuliyoyafanya.
Nyumba yetu ya Dar es salaam tuliwapa wazazi wangu. Biashara zangu zote nilizihamishia Marekani, mtoto wetu alianza shule huko Tressy nae akapata kazi ya moja kwa moja FBI, kila kitu kilienda vizuri.
Hata kabla hatujamaliza mwezi mmoja katika yale makazi yetu mapya wazazi wangu walinipigia simu.
“We miss you son” (tumekukumbuka mwanetu) waliniambia kwa upendo mkubwa wa kizazi.
“Dady and Mumy I Will be Back” (baba na mama nitarudi) niliwaambia kwa kudeka.
MWISHO
Nikiwa kama Mwandishi Hii Simulizi imenichuka Muda Mrefu Sana Kuitunga Yaani Karibu Mwezi Mzima, Lakini Kwa Kuwa nawajali mashabiki Zangu nimeitoa Kwenu Bureee Kabisa. Pia Ningependa Kujua Kwa Upande Wako Wewe Umechukua Siku Ngapi Kuimaliza Simulizi Hii Mapaka Mwisho?
Hapo Ndio Mwisho wa Simulizi yetu Hii ya I Will be Back. Kwa Simulizi za Kusisimua na Kufundisha Kama Hizi Endelea Kutembelea Africona.
- 97shares
- Facebook43
- Twitter54
- Gmail
- Copy Link