Hadithi yetu hii ya mtoto wa makame wa makame imehadithiwa na bibi Subira Abassi. Soma hadi mwisho Hadithi hii Utafahamu jinsi alivyo okoa kijiji chao.
HADITHI YA MTOTO WA MAKAME WA MAKAME
Hapo zamani za kale alikuwepo bwana mmoja akiitwa Makame wa Makame, akajenga nyumba na akatafuta mke akaowa. Walikaa na walibahatika kupata mtoto wa kiume. Waliendelea kuishi na wakatafuta paka wakafuga, na hatimae paka huyo akawa mkubwa na nunda na akawala watu wote pale kiamboni,
na zile nyumba za mtaani zikawa tupu, hazina watu, mpaka Makame wa Makame pia akaliwa, na alibakia yule mke mtu na mtoto wake tu.
Waliishi yule mtoto na mama yake siku moja mtoto alimuuliza mama yake „Mama mbona nyumba zote hizo haziishi watu?”. Mama mtu alimjibu mwanawe; „
Mwanangu we hapo zamani baba yako alikua anafuga paka sasa yule paka kageuka nunda na amewala watu wote mpaka baba yako ameliwa isipokuwa
sisi tu ndio hatukuliwa na paka huyo.”
Yule mtoto alimwambia mama yake atafutiwe vibuyu saba na manda saba, akatafutiwa vibuyu saba vya maji na manda saba na akapewa mshale wa baba yake. Mtoto huyo aliondoka na kuelekea mwituni, akaranda, siku ya kwanza, ya pili, ya tatu, ya nne, ya tano, ya sita hadi siku ya saba akamkuta kima akampiga alimchukua na alirudi nyumbani kwao huku akiimba.
Mama wee ndie huyu nunda mla watu eee mama Aliimba mpaka alipofika kwao alikua akiimba nyimbo hiyo. Na Mama mtu alimjibu mwanawe. Mwanangu wee sie huyo nunda mla watu watu eee mwana eee..
Baada ya siku mbili mtoto alimuagiza mama yake amtafutie vibuyu vyengine saba vya maji na manda saba, alipewa, akatoka akenda kule msituni akamkuta paa akampiga, akamchukua na kurudi kwao huku akiimba nyimbo.
Mama wee ndie huyu nunda mla watu eee mama Mama mtu akamjibu mwanawe. Mwanangu wee sie huyo nunda mla watu Alipofika akaambiwa siye. Akakaa siku mbili akapumzika. Hapo akasema, siji mpaka nije nae, akahangaika mpaka ikafika siku ya saba vilipomalizika vitu vyake, maji na manda, alimkuta mnyama mkubwa sana akampiga, akaenda nae na alipofika nyumbani akaanza kuimba.
”Mama wee ndie huyu nunda mla watu eee mama”
Na mama mtu akamjibu mwanawe.
Mwanangu wee ndie huyo nunda mla watu Hapo akamuweka mpaka asubuhi. Ilipofika asubuhi akatafutiwa chai na alipomaliza akauliza kisu cha baba kipo wapi? Akapewa kile kisu akampasua kwa bahati mbaya ndani ya lile tumbo alikuwemo baba yake akamtoga kisu cha jicho, hapo wakatoka watu wote aliowameza, ikisha wale watu waliuliza ilikuwaje?
Mama mtu akajibu; „alisema apewe mshale wa baba yake akamtafute huyo mnyama aliemeza watu, na huyu mtoto ndie aliekutafuteni hadi kufika hapa, kila mtu akaenda nyumbani kwake wakampa vitu walivyojaaliwa navyo.”
Na baba mtu akauliza kwa nini watu wote wametoka salama isipokuwa mimi nimetoka jicho moja?
Hapo watu akamuombea yule mtoto na akasamehewa.
MWISHO
Wangapi walisha wahi kusimuliwa Hadithi ya Mtoto wa makame wa makame au inayoendana na Hiyo.
Pia ni funzo gani umelipata katika Hadithi hii nzuri ya Kale. Niandikie Hapo chini kwenye Comment…
- 123shares
- Facebook67
- Twitter56
- Gmail
- Copy Link