in

SARAFINA: MOJA KATI YA SIMULUIZI PENDWA MNO

Simulizi ya Sarafina ni Moja Kati ya Simulizi Pendwa Mno Zenye Mafunzo MbaliMbali Katika Maisha. Mtunzi wa Simulizi Hii ni Mimi Kipenzi cha wapenda Simulizi @aisha-mapepe

Sarafina Simulizi

SIMULIZI YA SARAFINA

Ni miaka kumi na mbili tangu niiombe nafasi hii ya kukutana na wewe Sarafina, nimepitia kipindi kigumu cha kutamani kuingia katika nafsi yako walau ujue ni kiasi gani ninahitaji wakati kama huu.
Asante sana kwa nafasi hii Sarafina!

Haijawahi kutoka katika kumbukumbu zangu kuwa ulikuwa mwezi wa pili wakati inatambulika kuwa mama yako ni mjamzito. Nakiri kuwa hadi sasa sifahamu ni tarehe ipi rasmi uliyoingia ulimwenguni na kujikuta katika malezi ya upande mmoja. Najua fika umejilazimisha kuwa mbele yangu leo hii. Lakini angali masikio yako yapo wazi naamini unanisikiliza.

Siitumii nafasi hii kujitetea bali naitumia walau kuusema ukweli wa moyo wangu. Najua wazi kuwa mama yako amekujaza maneno ya chuki kuhusu mimi, amekulisha sumu na hata sasa unajitazama ukiwa umesimama mbele ya kiumbe kinachotisha sana.

*********

Sitaki kuzibadili fikra zako Sarafina, bali nahitaji kuusema ukweli tu! Yawezekana kweli kabisa nilikuwa baba mbaya, kwa sababu mama yako amekujenga hivyo.

Sarafina mwanangu, haikuwa rahisi mimi kumpata mama yako na hata nilivyompata ilikuwa ngumu sana kumuamini kama ni kweli ananipenda. Kama unavyoniona leo ndivyo ilivyokuwa wakati wetu….

sikuwa nikitoka jamii ya kitajiri, hata mama yako pia ilikuwa hivyo. Namshukuru Mungu mama yako amekuachia urembo wake wote….. Mama yako alijaliwa Urembo na kila mwenye jicho aliliona hilo.
Hiki ni mojawapo ya kitu ambacho kilimzuzua mama yako, karibia mara tatu aliwahi kuniambia kuwa hawezi kuolewa na mtu maskini.

Hicho kilikuwa ni kijembe kuja kwangu! Nilijitahidi kadri ya uwezo wangu kumpa mahitaji madogomadogo….. mama yako hakuridhika. AJABU ni kwamba, kile ambacho hakukipata kwangu alikipata alipojua yeye na hakutaka maswali. Nikawa mpole, hata nikimwambia akirudishe mimi nitatoa wapi pesa ya kukinunua?

Kumbi za Disko zikaanza kumzoea, sikuipenda tabia yake hii na nilimweleza wazi kuwa sio maisha ambayo ni chaguo letu. Akakubali kuwa atabadilika….. lakini haikuwa hivyo.

Siku iliyobadili mambo yote ni ile ambayo nilijaribu kumfuatilia na kugundua kuwa ameenda katika kumbi za disko. Sarafina, baba yako naye ni mwanadamu….

Nilipandwa na jazba sana baada ya mama yako kusema kuwa mimi ninamuonea wivu kwa sababu sina kiingilio cha kumudu kuingia katika kumbi hizo, akaongezea neno la kukera kuwa kama nitahitaji kuingia basi niende atanilipia.

*********

Hakika nilighadhabika, nikafyatuka na kumnasa kofi moja shavuni akaanguka chini.
Kuanzia hapo hakutaka amani wala upatanisho na mimi.

Baada ya mwezi mmoja wa ukimya akarejea kwangu kunieleza kuwa ni mjamzito, nilistaajabu sana. Sikustaajabu kwa sababu ya ule ujauzito bali ni katika namna aliyonipa taarifa….
Alikuwa kama anayenifokea na hapohapo akanieleza kuwa napaswa kumuhudumia yeye na tumbo lake kama sifanyi hivyo atanishtaki.

Mwanangu Sarafina, hakuna kitu baba yako nakiogopa hadi leo kama masuala ya polisi, sitaki kabisa kupasikia. Nawe nakusihi sana upaogope huko, hata ikitokea umekorofishana na mtu tafadhali tazama kwanza namna ya kwanza ya kuleta suluhu kabla haujakimbilia polisi.

Nikamuuliza mama yako, kwa nini asiketi tuzungumze, akanitazama kisha akasonya.
Nikaona anatoa simu ya mkononi, nakumbuka ilikuwa mwishoni mwa miaka ya 1999 kuelekea 2000 wakati huo simu za mkononi zikiwa ni jambo la anasa sana nchini kwetu.
Ukiwa na simu ile basi jamii inakutazama kama mtu uliyeyaweza maisha tayari.
Mama yako na umasikini ule alikuwa ameitoa wapi?
Nikajikuta ninamuuliza…. hilo nalo likawa kosa.

Alinitukana sana…..
Nikamuuliza swali dogo tu…..
Huo ujauzito una miezi mingapi?
Mama yako akanicharua kuwa ninaikataa mimba.
Sarafina sikuwahi kukukana, kama masikio yako yalikuwa wazi wakati haya yanatokea naamini ulisikia na ndo maana leo upo hapa mwanangu.

Kuanzia hapo ugeni wa shari ukawa hauishi nyumbani kwangu, leo atakuja rafiki yake na kuniambia sarafina anataka kwenda hospitali maana anatapika sana, kesho anakuja anayejitambulisha kama shangazi yake Sarafina na kunieleza kuwa mama yako anatakiwa kuanza kliniki, na hapo ananitajia gharama.

*********

Vingine vilikuwa ni vichekesho vinavyoudhi sana….
Eti anakuja mama mdogo anasema kuwa natakiwa nitoe pesa ya nguo za mtoto…
Sarafina kweeeli! Nguo zako nizinunue angali una mwezi na kitu tumboni.
Kama sio kunikomoa ni kitu gani hiki mama yako alinifanyia….
Na hapo nikiwa bado naumizwa kichywa na ukweli wa lile jambo kuwa ile mimba ni yangu ama kuna mwingine. Kama nilivyokwambia mama yako uzuri ulikuwa unamzuzua…..
Je? huyo aliyempatia simu ya mkononi aliondoka patupu?
Sisemi umtambue mama yako kama malaya. La!
Hayo ya kutambua kama ni malaya ama la tuachie sisi, tulitambuana tulivyoweza….. kadiri ya hisia zetu zilipotutuma.

Kama mama yako alikuwa na nia ya kunikomoa, hakika aliniweza. nilikonda sana. Kila nikisikia hodi najua ni ujumbe kutoka kwa mama yako. sikuwa naweza kulala vizuri, nikalazimika kufanya kazi ambazo zinahatarisha afya yangu ili kuvuna kipato cha ziada ili mama yako aridhike na kila mjumbe wake apate ambalo anahitaji.

Raisi aliyekuwa madarakani wakati wa majanga haya alikuwa ni Benjamin William Mkapa, huyu raisi hakuwa mchezo na haki za akina mama. Na juu ya hilo kuna mkutano mkubwa sana ulikuwa umefanyika mwaka 1995, umesoma mwanangu na ninaamini umekisikia kitu kilichoitwa BEIJING CONFERENCE, Mkutano wa akina mama kusimamia haki zao.

*********

Hivyo kwa wakati huo mama akikohoa tu, mwanaume unapigwa mijeledi.
Mwanangu nilikuwa muoga sana, na uoga wangu ukanifanya nichukue maamuzi ya kukimbilia mkoani Mbeya na kisha nchini Malawi kupambana nipate pesa.
Niliamini kuwa nikiwa na pesa mama yako ataniheshimu, hao mashangazi, kina mamdogo hawataongea nami kama waongeavyo na mbwa mzee.
Niliamini kuwa pesa ina nguvu ya kumsahaulisha mama yako hata juu ya huo mkutano wa Beijing.

Nilipambana nilivyoweza lakini sikufanikiwa kufikisha huduma yoyote kwa mama yako kwa sababu ya kutokuwa na mawasiliano naye.
Lakini sikuwa mjinga wa kungoja mawasiliano nd’o nikuhudumie mwanangu… nilikuwa nakufikiria siku zote. Sijui aliyekupa jina la Sarafina, lakini hakika linanipendeza sana….

Nilikutambulisha kwa kila aliyenifahamu, nikawaeleza kuwa ninaye mtoto mmoja, kuna wengine niliwaeleza kuwa ni mtoto wa kiume na wengine nikawaambia ni wa kike.
Nilichotaka ni wao kutambua kuwa ninaye mtoto.

Mwanangu nimesema mengi sana, na wala sihitaji kusema mengi zaidi. Nakuomba uchukue hiyo bahasha hapo mezani. katika kutafuta kwangu nilifanikiwa kununua hekari mbili za mashamba ya miti ainja ya mitiki huko Mufindi…..

*********

Sikuwa najua jina lako wala jinsia niliandika kuwa shamba hili ni ali ya mwanangu. na huyo mtoto ni wewe, huu ndo urithi niliokuandalia. Ukiuza shamba hili utapata mamilioni ya Pesa, yatakayo kuvusha katika madaraja ya Elimu kadri ya uhitaji wako.

Asante kwa kuitikia wito Sarafina, ukionana na mama yako mwambie kuwa MIMI NIPO! na sina mtoto zaidi yako SARAFINA

MWISHO

Katika simulizi hii umeweza kuona jinsi wazazi wanavyosambaza chuki kwa watoto na kuleta mpasuko. Zaidi umeona nguvu ya mali na pesa kiujumla katika mapenzi. Lakini Je, IPO WAPI NGUVU YA MSAMAHA!!!

Ndugu Msomaji, ukipata Nafasi ya kusamehe Tafadhali Samehe.

ASANTE!

Written by Aisha Mapepe

Aisha Mapepe ni Mwandishi wa Simulizi Mbalimbali za Mapenzi, Maisha na za Kuelimisha. Lengo ni Kuburudisha Jamii na Kuondoa Stress za Maisha zinazo tukabili Baadhi Yetu.

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Amka Mama

AMKA MAMA: SIMULIZI YA KUSISIMUA NA KUHUZUNISHA

Ashura Sio Mtu Mzuri

ASHURA SIMULIZI: Kweli Ashula Sio Mtu Mzuri